Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) leo (Disemba 5, 2017) imetangaza orodha yenye wanafunzi 2,679 ambao wamepata mikopo ya elimu ya juu yenye thamani ya TZS 9.6 bilioni kufuatia kukamilika kwa uchambuzi wa rufaa zilizowasilishwa na wanafunzi hao.
Kati ya wanafunzi hao, 1,847 ni wa mwaka wa kwanza ambao mikopo yao ina thamani ya TZS 6.84 bilioni na wengine 832
ni wale wanaoendelea na masomo lakini hawakuwa na mikopo katika miaka
iliyopita. Wanafunzi hao wanaoendelea na masomo wamepata mikopo yenye
thamani ya TZS 2.76 bilioni.
Orodha kamili ya wanafunzi waliofanikiwa kupata mikopo kupitia dirisha la rufaa pamoja na fedha za wanafunzi hao zimetumwa katika vyuo walipo wanafunzi hao hivi sasa.
KUFUNGUA ORODHA HIYO
Hatua hii inafanya jumla ya wanafunzi 33,200 wa mwaka wa kwanza kuwa wamepangiwa mikopo yenye thamani ya zaidi ya TZS 108 bilioni kwa mwaka wa masomo 2017/2018 hadi sasa. Bajeti ya jumla kwa wanafunzi wote kwa mwaka 2017/2018 ni TZS 427.54 bilioni.
Dirisha
la rufaa lilifunguliwa kwa siku saba kuanzia tarehe 13 Novemba, 2017
hadi tarehe 19 Novemba, 2017 ili kuwapa fursa waombaji wote ambao
hawakuwa wameridhika na upangaji wa mikopo na kuwasilisha rufaa kupitia
vyuo walivyopata udahili.
Wanafunzi waliohamishiwa mikopo yao
Wakati huohuo,
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imeanza kuhamisha mikopo
iliyokuwa imeelekezwa katika vyuo tofauti na waliko kwa sasa. Mikopo ya
wanafunzi 590 wa mwaka wa kwanza yenye thamani ya TZS 1.78 bilioni ambayo awali ilikuwa imepelekwa katika vyuo tofauti na walipo wanafunzi imehamishwa.
Wanafunzi
hao waliohamishiwa mikopo yao ni wale ambao walipangiwa mikopo na
kupelekewa fedha zao katika vyuo ambavyo walipata udahili awali, ila
baadaye wakaamua kujiunga na vyuo vingine ambavyo nako walipata udahili.
Orodha kamili ya wanafunzi hao pamoja na fedha za wanafunzi hao zimetumwa katika vyuo walipo hivi sasa.
Bodi
ya Mikopo inaendelea kupokea orodha za wanafunzi waliosajiliwa katika
vyuo mbalimbali na wale wenye mikopo, fedha zao zitahamishiwa katika
vyuo walipo katika awamu zijazo.
Mikopo kwa Wahadhiri wa Vyuo Vikuu
Aidha, jumla ya wanafunzi 45 wa shahada za uzamili na uzamivu ambao ni wanataaluma na waajiriwa wa vyuo mbalimbali nchini wamepata mikopo yenye thamani ya TZS 441.4 milioni katika mwaka wa masomo 2017/2018.
Mikopo
hii hutolewa na Bodi ya Mikopo kwa wanataaluma hao ili kuvijengea vyuo
uwezo wa kitaaluma chini ya makubaliano kati ya Bodi ya Mikopo na vyuo
hivyo.
Imetolewa na:
Abdul-Razaq Badru
MKURUGENZI MTENDAJI
BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU
Jumanne, Disemba 5, 2017
Post a Comment